1. Na mtu atakapomtolea BWANA matoleo ya sadaka ya unga, matoleo yake yatakuwa ya unga mwembamba; naye ataumiminia mafuta, na kutia na ubani juu yake;
2. kisha atauleta kwa wana wa Haruni, hao makuhani; naye atatwaa konzi moja katika huo unga mwembamba, na katika mafuta yake, na huo ubani wote; kisha kuhani atauteketeza kuwa ndio ukumbusho wake juu ya madhabahu, ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA;
3. na huo uliosalia wa ile sadaka ya unga utakuwa ni wa Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.
4. Tena, utakapotoa matoleo ya sadaka ya unga uliookwa tanuuni, yatakuwa mikate isiyotiwa chachu, ya unga mwembamba uliokandwa na mafuta, au maandazi yasiyochachwa yaliyopakwa mafuta.