Law. 18:2-16 Swahili Union Version (SUV)

2. Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

3. Nanyi msifanye matendo kama yale ya nchi ya Misri mliyokaa; wala msifanye matendo kama yale ya nchi ya Kanaani, nitakayowapeleka; wala msiende katika amri zao hao.

4. Mtazifanya hukumu zangu, nanyi mtazishika amri zangu, ili mwenende katika hizo; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

5. Kwa ajili ya hayo mtazishika amri zangu na hukumu zangu; ambazo mtu akizitumia ataishi kwa hizo; mimi ndimi BWANA.

6. Mtu ye yote aliye wa kwenu asimkaribie mwenziwe aliye wa jamaa yake ya karibu ili kumfunua utupu; mimi ndimi BWANA.

7. Utupu wa baba yako, wala utupu wa mama yako, usifunue, maana ndiye mama yako; usifunue utupu wake.

8. Utupu wa mke wa baba yako, usifunue; maana, ni utupu wa baba yako.

9. Utupu wa umbu lako, binti ya baba yako, au binti ya mama yako, kwamba alizaliwa nyumbani mwenu au kwamba alizaliwa kwengine, utupu wa hao usifunue.

10. Utupu wa binti ya mwanao mume, au wa binti ya binti yako, utupu wao hao usifunue; kwa kuwa ndio utupu wako mwenyewe.

11. Utupu wa binti ya mkewe baba yako, aliyezaliwa na baba yako, yeye ni umbu lako, usifunue utupu wake.

12. Usifunue utupu wa umbu lake baba yako; maana, yeye ni jamaa aliye karibu.

13. Usifunue utupu wa umbu la mama yako; maana, yeye ni jamaa ya mama yako ya karibu.

14. Usifunue utupu wa ndugu ya baba yako, usimkaribie mkewe huyo; yeye ni shangazi lako.

15. Usifunue utupu wa mkweo mwanamke; yeye ni mke wa mwanao; usifunue utupu wake huyo.

16. Usifunue utupu wa mke wa nduguyo; maana, ni utupu wa nduguyo.

Law. 18