17. Usifunue utupu wa mwanamke na binti yake; usimtwae binti ya mwanawe mume, au binti ya binti yake, ili kufunua utupu wake; hao ni jamaa ya karibu; ni uovu mkuu.
18. Wala usitwae mwanamke pamoja na nduguye, awe mtesi wake, na kufunua utupu wake, huyo wa pili atakapokuwa yu hai.
19. Nawe usimkaribie mwanamke kufunua utupu wake wakati wa kutengwa kwa ajili ya unajisi wake.
20. Usilale na mke wa mwenzio, ukajitia unajisi naye.
21. Nawe usitoe kizazi chako cho chote na kuwapisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la Mungu wako; mimi ndimi BWANA.
22. Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo.
23. Wala usilale na mnyama ye yote, ili kujitia unajisi kwake; wala mwanamke asisimame mbele ya mnyama ili kulala naye; ni uchafuko.
24. Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote;
25. na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa.
26. Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu;
27. (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;)
28. ili kwamba hiyo nchi isiwatapike na ninyi pia, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu.
29. Kwani mtu awaye yote atakayefanya machukizo hayo mojawapo, nafsi hizo zitakazoyafanya zitakatiliwa mbali na watu wao.