1. BWANA akasema na Musa, baada ya kufa kwa hao wana wawili wa Haruni, walipokaribia mbele za BWANA, wakafa;
2. BWANA akamwambia Musa, Sema na Haruni ndugu yako, kwamba asiingie wakati wo wote katika mahali patakatifu ndani ya pazia, mbele ya kiti cha rehema, kilicho juu ya sanduku, asije akafa; maana, mimi nitaonekana katika lile wingu juu ya kiti cha rehema.
3. Haruni ataingia katika patakatifu na vitu hivi; ng’ombe mume mchanga kwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa.
4. Ataivaa ile kanzu takatifu ya kitani, atakuwa na zile suruali za kitani mwilini mwake, atafungwa ule mshipi wa kitani, naye atavaa ile kofia ya kitani; hayo ndiyo mavazi matakatifu, naye ataoga mwili wake majini, na kuyavaa.
5. Kisha atatwaa mikononi mwa mkutano wa Waisraeli mbuzi waume wawili, kwa sadaka ya dhambi; na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa.
6. Na Haruni atamtoa yule ng’ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake.
7. Kisha atawatwaa wale mbuzi wawili na kuwaweka mbele za BWANA mlangoni pa hema ya kukutania.
8. Na Haruni atapiga kura juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya BWANA; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli.
9. Na Haruni atamleta yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya BWANA, na kumtoa awe sadaka ya dhambi.
10. Bali yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya Azazeli atawekwa hai mbele za BWANA ili kumfanyia upatanisho, ili kumpeleka jangwani kwa ajili ya Azazeli.
11. Na Haruni atamsongeza ng’ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake; naye atamchinja yule ng’ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake.
12. Kisha atatwaa chetezo kilichojaa makaa ya moto yatokayo katika madhabahu iliyo mbele za BWANA, na konzi mbili za uvumba mzuri uliopondwa sana, mikononi mwake, naye atauleta ndani ya pazia.
13. Kisha atatia ule uvumba juu ya moto mbele za BWANA, ili moshi wa ule uvumba ukisitiri kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, asije akafa.
14. Kisha atatwaa baadhi ya damu ya yule ng’ombe, na kuinyunyiza kwa kidole chake juu ya kiti cha rehema upande wa mashariki; na mbele ya kiti cha rehema atainyunyiza ile damu kwa kidole chake mara saba.
15. Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya vile vile kama alivyofanya kwa damu ya ng’ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema,
16. naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao.
17. Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli.