Law. 14:6-19 Swahili Union Version (SUV)

6. kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya hivyo, pamoja na yule ndege aliye hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni;

7. kisha atamnyunyizia huyo atakayetakaswa na ukoma mara saba, naye atasema kwamba yu safi, kisha atamwacha yule ndege aliye hai aende zake nyikani.

8. Naye huyo atakayetakaswa atazifua nguo zake, na kunyoa nywele zake zote, na kuoga katika maji, naye atakuwa safi; baada ya hayo ataingia ndani ya marago, lakini ataketi nje ya hema yake muda wa siku saba.

9. Kisha siku ya saba atanyoa nywele zote za kichwani mwake, na ndevu zake, na nyushi zake, nywele zake zote pia atazinyoa; kisha atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa safi.

10. Kisha siku ya nane atachukua wana-kondoo wawili waume wakamilifu, na mwana-kondoo mmoja wa kike wa mwaka wa kwanza mkamilifu, na sehemu tatu za kumi za efa moja ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, kuchanganywa na mafuta, na logi moja ya mafuta.

11. Kisha kuhani atakayemtakasa atamsimamisha huyo mtu atakayetakaswa, pamoja na vitu vile vyote, mbele za BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania;

12. kisha kuhani atamshika mmoja katika hao wana-kondoo waume, na kumsongeza awe sadaka ya hatia, pamoja na hiyo logi ya mafuta, kisha atavitikisa kuwa ni sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA;

13. kisha atamchinja huyo mwana-kondoo mahali hapo wachinjapo sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, ndani ya mahali patakatifu; kwa kuwa kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo ya kuhani, ni vivyo sadaka ya hatia; ni takatifu sana;

14. kisha huyo kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya hatia, naye kuhani ataitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume;

15. kisha kuhani atatwaa katika hiyo logi ya mafuta, na kuyamimina katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto;

16. kisha kuhani atatia kidole cha mkono wa kuume katika hayo mafuta, yaliyo katika mkono wake wa kushoto, naye atayanyunyiza hayo mafuta kwa kidole chake mara saba mbele za BWANA;

17. na katika yale mafuta yaliyobaki mkononi mwake kuhani atayatia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya damu ya sadaka ya hatia;

18. na mafuta yaliyobaki, yaliyo katika mkono wa kuhani, atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, mbele za BWANA.

19. Kisha kuhani atasongeza sadaka ya dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa kwa sababu ya unajisi wake; kisha baadaye ataichinja sadaka ya kuteketezwa;

Law. 14