Law. 14:41-57 Swahili Union Version (SUV)

41. naye atafanya kwamba hiyo nyumba ikwanguwe ndani pande zote, na chokaa watakayokwangua wataimwaga nje ya mji mahali palipo na uchafu;

42. kisha watatwaa mawe mengine, na kuyatia mahali pa mawe hayo; naye atatwaa chokaa nyingine, na kuipaka chokaa hiyo nyumba.

43. Na kama hilo pigo likirudi tena, na kutokea ndani ya nyumba, baada ya yeye kuyatoa hayo mawe, na baada ya kuikwangua nyumba, na baada ya kupakwa chokaa,

44. ndipo kuhani ataingia ndani na kuangalia, na tazama, likiwa pigo limeenea ndani ya hiyo nyumba, ni ukoma unaokula hiyo nyumba; ni katika unajisi.

45. Naye ataibomoa nyumba, mawe yake, na miti yake, na chokaa yote ya hiyo nyumba; naye atavichukua vyote nje ya mji hata mahali palipo na uchafu.

46. Tena mtu atakayeingia ndani ya hiyo nyumba wakati huo wote iliofungwa, atakuwa najisi hata jioni.

47. Na mtu alalaye ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake, naye alaye chakula ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake.

48. Tena kwamba kuhani akiingia ndani na kuangalia, na tazama, ikiwa pigo halikuenea katika hiyo nyumba, baada ya nyumba kupakwa chokaa; ndipo kuhani atasema kwamba hiyo nyumba i safi, maana, pigo limepoa.

49. Naye atatwaa ndege wawili, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo, kwa kuitakasa hiyo nyumba;

50. naye atamchinja mmojawapo wa ndege hao katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni;

51. kisha atatwaa huo mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, pamoja na huyo ndege aliye hai, na kuvichovya vyote katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa, na katika hayo maji ya mtoni, na kuinyunyiza nyumba mara saba;

52. naye ataitakasa hiyo nyumba kwa damu ya ndege, na kwa maji ya mtoni, na kwa huyo ndege aliye hai, na kwa mti wa mwerezi, na kwa hisopo, na kwa sufu nyekundu;

53. lakini ndege aliye hai atamwacha atoke mle mjini aende nyikani; ndivyo atakavyofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo nyumba; nayo itakuwa safi.

54. Hiyo ndiyo sheria ya pigo la ukoma ya kila aina, na ya kipwepwe;

55. na ya ukoma wa vazi, na ukoma wa nyumba;

56. na kivimbe, na kikoko na kipaku king’aacho;

57. ili kufunza itakapokuwa ni unajisi, na itakapokuwa ni safi; hiyo ndiyo sheria ya ukoma.

Law. 14