21. Tena kwamba ni maskini, naye hawezi kupata kiasi hicho, ndipo atatwaa mwana-kondoo mmoja wa kiume, awe sadaka ya hatia ya kutikiswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake, na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga, na logi ya mafuta;
22. na hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kama awezavyo kuwapata; huyo mmoja atakuwa sadaka ya dhambi, na wa pili atakuwa sadaka ya kuteketezwa.
23. Hata siku ya nane atawaleta kwa kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania mbele za BWANA, kwa ajili ya kutakaswa kwake.
24. Na kuhani atamtwaa huyo mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na hiyo logi ya mafuta, naye kuhani atavitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA;
25. kisha atamchinja mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na kuhani atatwaa katika damu ya sadaka ya hatia, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume;
26. kisha kuhani atamimina sehemu ya hayo mafuta katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto;
27. kisha kuhani atanyunyiza baadhi ya hayo mafuta yaliyo katika mkono wake wa kushoto, kwa kidole chake cha mkono wa kuume mara saba mbele za BWANA;
28. kisha kuhani atatia mengine katika hayo mafuta yaliyo mkononi mwake katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya mahali pale penye damu ya sadaka ya hatia;
29. na mafuta yaliyobaki katika mkono wa kuhani atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA.
30. Kisha atasongeza hao hua mmojawapo, au hao makinda ya njiwa mmojawapo, kadiri ya awezao kuwapata;
31. hata kadiri aliyoweza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya unga; na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa mbele za BWANA.
32. Huyo ambaye ndani yake mna pigo la ukoma, ambaye hawezi kukipata hicho kipasacho kutakaswa kwake, sheria yake ni hiyo.
33. BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
34. Hapo mtakapoingia nchi ya Kanaani, ambayo nawapa kuwa ni milki yenu, nami nitakapolitia pigo la ukoma katika nyumba ya nchi hiyo ya milki yenu;
35. ndipo mwenye nyumba hiyo atakwenda na kumwambia kuhani, akisema, Naona mimi ya kwamba pana kama pigo katika nyumba yangu;