12. kisha kuhani atamshika mmoja katika hao wana-kondoo waume, na kumsongeza awe sadaka ya hatia, pamoja na hiyo logi ya mafuta, kisha atavitikisa kuwa ni sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA;
13. kisha atamchinja huyo mwana-kondoo mahali hapo wachinjapo sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, ndani ya mahali patakatifu; kwa kuwa kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo ya kuhani, ni vivyo sadaka ya hatia; ni takatifu sana;
14. kisha huyo kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya hatia, naye kuhani ataitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume;
15. kisha kuhani atatwaa katika hiyo logi ya mafuta, na kuyamimina katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto;
16. kisha kuhani atatia kidole cha mkono wa kuume katika hayo mafuta, yaliyo katika mkono wake wa kushoto, naye atayanyunyiza hayo mafuta kwa kidole chake mara saba mbele za BWANA;
17. na katika yale mafuta yaliyobaki mkononi mwake kuhani atayatia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya damu ya sadaka ya hatia;