1. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2. Hii ndiyo sheria ya mwenye ukoma, katika siku ya kutakaswa kwake; ataletwa kwa kuhani,
3. na huyo kuhani atatoka aende nje ya marago; na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pigo la ukoma limepoa kwake huyo mwenye ukoma;
4. ndipo huyo kuhani ataagiza kwamba watwae kwa ajili yake atakayetakaswa ndege wawili walio hai, ambao ni safi, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo;
5. kisha kuhani ataagiza ndege mmoja achinjwe katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni;
6. kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya hivyo, pamoja na yule ndege aliye hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni;
7. kisha atamnyunyizia huyo atakayetakaswa na ukoma mara saba, naye atasema kwamba yu safi, kisha atamwacha yule ndege aliye hai aende zake nyikani.