9. Pigo la ukoma litakapokuwa katika mtu, ndipo ataletwa kwa kuhani;
10. na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pana kivimbe cheupe katika ngozi yake, na malaika yamegeuzwa kuwa meupe, tena ikiwa pana nyama mbichi iliyomea katika kile kivimbe,
11. ni ukoma wa zamani ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa yu najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye yuna unajisi.
12. Tena kwamba huo ukoma ukitokeza katika ngozi yake, na ukoma ukamwenea ngozi yote, tangu kichwa hata miguuni, kama aonavyo kuhani;
13. ndipo huyo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa yu safi huyo aliye na hilo pigo umegeuka kuwa mweupe wote; yeye ni safi.
14. Lakini po pote itakapoonekana nyama mbichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi.
15. Kuhani ataiangalia hiyo nyama mbichi, naye atasema kuwa yu najisi; ile nyama mbichi ni najisi; ni ukoma.
16. Au kama hiyo nyama mbichi iligeuka tena, na kugeuzwa kuwa nyeupe, ndipo atamwendea kuhani,
17. na huyo kuhani atamwangalia; na tazama, ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa yu safi huyo aliyekuwa na pigo; yeye yu safi.
18. Tena mwili wa mtu utakapokuwa na jipu katika ngozi yake, nalo limepoa,
19. na mahali palipokuwa na lile jipu pana kivimbe cheupe, au kipaku king’aacho, cheupe lakini chekundu kidogo, ndipo atamwonyesha kuhani mahali hapo;
20. na kuhani ataangalia, na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na malaika yakiwa yamegeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; ni pigo la ukoma limetokea katika hilo jipu.
21. Lakini kuhani akipaangalia, na tazama hamna malaika meupe ndani yake, wala hapana pa kuingia ndani kuliko ile ngozi, lakini paanza kufifia, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;
22. na kwamba pameenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo.
23. Lakini ikiwa kipaku hicho king’aacho kimeshangaa pale pale, wala hakienei, ni kovu ya jipu; na kuhani atasema kwamba yu safi.