5. kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limeshangaa, na pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena;
6. kisha siku ya saba kuhani atamwangalia tena; na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, wala pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atasema kuwa yu safi; ni kikoko; naye atazifua nguo zake, kisha atakuwa yu safi.
7. Lakini kwamba kikoko kimeenea katika ngozi yake baada ya kuonyesha nafsi yake kwa kuhani kwa kupata kutakaswa kwake ataonyesha nafsi yake tena kwa kuhani;
8. na kuhani ataangalia, na tazama ikiwa hicho kikoko kimeenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kuwa yu najisi; ni ukoma.
9. Pigo la ukoma litakapokuwa katika mtu, ndipo ataletwa kwa kuhani;
10. na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pana kivimbe cheupe katika ngozi yake, na malaika yamegeuzwa kuwa meupe, tena ikiwa pana nyama mbichi iliyomea katika kile kivimbe,
11. ni ukoma wa zamani ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa yu najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye yuna unajisi.
12. Tena kwamba huo ukoma ukitokeza katika ngozi yake, na ukoma ukamwenea ngozi yote, tangu kichwa hata miguuni, kama aonavyo kuhani;
13. ndipo huyo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa yu safi huyo aliye na hilo pigo umegeuka kuwa mweupe wote; yeye ni safi.
14. Lakini po pote itakapoonekana nyama mbichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi.
15. Kuhani ataiangalia hiyo nyama mbichi, naye atasema kuwa yu najisi; ile nyama mbichi ni najisi; ni ukoma.
16. Au kama hiyo nyama mbichi iligeuka tena, na kugeuzwa kuwa nyeupe, ndipo atamwendea kuhani,
17. na huyo kuhani atamwangalia; na tazama, ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa yu safi huyo aliyekuwa na pigo; yeye yu safi.