32. Tena kitu cho chote, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, wakiisha kufa, kitakuwa ni najisi; kwamba ni chombo cha mti, au nguo, au ngozi, au gunia, chombo cho chote kitakachoangukiwa, ambacho ni chombo cha kufanyia kazi yo yote, lazima kitiwe ndani ya maji, nacho kitakuwa ni najisi hata jioni; ndipo kitakapokuwa ni safi.
33. Na kila chombo cha udongo, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, kila kilichomo ndani yake kitakuwa ni najisi, na hicho chombo kitavunjwa.
34. Kila chakula kilichomo, ambacho ni kuliwa, hicho ambacho maji hutumiwa juu yake, kitakuwa ni najisi; na kila kinyweo ambacho ni cha kunywewa, kilichomo katika chombo kama hicho, kitakuwa ni najisi.
35. Na kila kitu kitakachoangukiwa na kipande cho chote cha mizoga yao kitakuwa najisi; kwamba ni tanuru, au meko ya vyungu, kitavunjwa vipande vipande; ni najisi vitu hivyo, navyo vitakuwa najisi kwenu.
36. Pamoja na hayo, chemchemi, au shimo, ambamo maji yakusanyika, vitakuwa ni safi; lakini hicho kitakachogusa mizoga yao kitakuwa ni najisi.
37. Na kipande cho chote cha mzoga kikiwa kimeangukia mbegu za kupandwa zitakazopandwa, zitakuwa safi.
38. Lakini kwamba hizo mbegu zilitiwa maji na cho chote cha mizoga yao kuziangukia, ni najisi kwenu.
39. Kama akifa mnyama awaye yote, ambaye mna ruhusa kumla, yeye anayeugusa mzoga wake atakuwa najisi hata jioni.
40. Na yeye atakayekula nyama ya mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; yeye atakayeuchukua mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hata jioni.
41. Na kila kitu kitambaacho juu ya nchi ni machukizo; hakitaliwa.
42. Kila aendaye kwa tumbo lake, na kila aendaye kwa miguu minne, na kila aendaye kwa miguu mingi, maana, ni vyote vyenye kutambaa vitambaavyo juu ya nchi, hamtavila, kwa kuwa ni machukizo.
43. Msifanye nafsi zenu kuwa ni chukizo kwa kitu cho chote chenye kutambaa, kitambaacho, wala msifanye nafsi zenu kuwa ni najisi kwa vitu hivyo, mkajipatia uchafu kwa hivyo.
44. Kwa kuwa mimi ni BWANA, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yo yote, kiendacho juu ya nchi.
45. Kwa kuwa mimi ni BWANA niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu.