22. katika hao mna ruhusa kuwala; nzige kwa aina zake, na nzige kuu kwa aina zake, na panzi kwa aina zake, na parare kwa aina zake.
23. Lakini vyote vitambaavyo vyenye mabawa, vilivyo na miguu minne, ni machukizo kwenu.
24. Nanyi mtakuwa najisi kwa wanyama hao; kila atakayegusa mzoga wao atakuwa ni najisi hata jioni;
25. na mtu awaye yote atakayechukua cho chote cha mizoga yao atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni.
26. Kila mnyama aliyepasuliwa ukwato, naye hana kwato mbili, wala hacheui, huyo ni najisi kwenu; kila agusaye wanyama hao atakuwa ni najisi.
27. Tena kila mnyama aendaye kwa vitanga vyake, katika hao wanyama wote waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu; awaye yote atakayegusa mizoga yao, atakuwa ni najisi hata jioni.
28. Na huyo atakayechukua mzoga wa wanyama hao atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hata jioni; hao ni najisi kwenu
29. Tena katika vitu vile vitambaavyo, vitambaavyo juu ya nchi, hivi ni najisi kwenu; kicheche, na panya, na mjombakaka, kwa aina zake,
30. na guruguru na kenge, na mjusi na goromoe, na lumbwi.
31. Wanyama hao ndio walio najisi kwenu katika hao watambaao; awaye yote atakayewagusa, wakiisha kufa, atakuwa ni najisi hata jioni.
32. Tena kitu cho chote, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, wakiisha kufa, kitakuwa ni najisi; kwamba ni chombo cha mti, au nguo, au ngozi, au gunia, chombo cho chote kitakachoangukiwa, ambacho ni chombo cha kufanyia kazi yo yote, lazima kitiwe ndani ya maji, nacho kitakuwa ni najisi hata jioni; ndipo kitakapokuwa ni safi.
33. Na kila chombo cha udongo, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, kila kilichomo ndani yake kitakuwa ni najisi, na hicho chombo kitavunjwa.