1. Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza.
2. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, nao ukawala, nao wakafa mbele za BWANA.
3. Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya.
4. Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjombaye Haruni, na kuwaambia, Njoni karibu, mwachukue hawa ndugu zenu, mkawaondoe hapa mbele ya maskani, mwende nao nje ya marago.
5. Basi wakaja karibu, na kuwachukua, hali wamevaa nguo zao, wakawachukua nje ya marago; kama Musa alivyosema.