6. Basi Haruni akaunyosha mkono wake juu ya maji yote ya Misri; na hao vyura wakakwea juu, wakaifunika nchi ya Misri.
7. Waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na kuwaleta vyura juu ya nchi ya Misri.
8. Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni BWANA, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee BWANA dhabihu.
9. Musa akamwambia Farao, Haya, ujitukuze juu yangu katika jambo hili; sema ni lini unapotaka nikuombee wewe, na watumishi wako, na watu wako, ili hao vyura waangamizwe watoke kwako wewe na nyumba zako, wakae ndani ya mto tu.
10. Akamwambia, Kesho, Akasema, Na yawe kama neno lako; ili upate kujua ya kwamba hapana mwingine mfano wa BWANA, Mungu wetu.
11. Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu.
12. Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia BWANA katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.
13. BWANA akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba.
14. Wakawakusanya chungu chungu; na nchi ikatoa uvundo.
15. Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama BWANA alivyonena.
16. BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri.
17. Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.
18. Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama.
19. Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.