Kut. 8:22-32 Swahili Union Version (SUV)

22. Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.

23. Nami nitatia mpaka kati ya watu wangu na watu wako; ishara hiyo italetwa kesho.

24. BWANA akafanya; wakaja wingi wa mainzi kwa uzito sana, wakaingia nyumbani mwa Farao, na katika nyumba za watumishi wake, tena katika nchi yote ya Misri; nayo nchi iliharibiwa kwa ajili ya wale mainzi.

25. Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii.

26. Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka BWANA, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe?

27. La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu BWANA, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza.

28. Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu BWANA, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni.

29. Musa akasema, Tazama, mimi natoka kwako, nami nitamwomba BWANA ili hao mainzi wamtoke Farao, na watumishi wake, na watu wake kesho; lakini Farao asitende kwa udanganyifu tena, kwa kutowaacha watu waende kumchinjia BWANA dhabihu.

30. Musa akatoka kwa Farao, akamwomba BWANA.

31. BWANA akafanya kama neno la Musa, akawaondoa wale mainzi wabaya kwake Farao, na kwa watumishi wake, na watu wake; hakusalia hata mmoja.

32. Farao akaufanya moyo wake kuwa mzito mara hiyo nayo, wala hakuwapa ruhusa hao watu waende zao.

Kut. 8