11. Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu.
12. Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia BWANA katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.
13. BWANA akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba.
14. Wakawakusanya chungu chungu; na nchi ikatoa uvundo.
15. Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama BWANA alivyonena.
16. BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri.
17. Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.
18. Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama.
19. Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.