7. Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao.
8. BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia,
9. Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka.
10. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.
11. Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.
12. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.
13. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena.
14. BWANA akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao.