Kut. 4:21-31 Swahili Union Version (SUV)

21. BWANA akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao.

22. Nawe umwambie Farao, BWANA asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu;

23. nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako.

24. Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua.

25. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi.

26. Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri.

27. BWANA akamwambia Haruni, Nenda jangwani uonane na Musa. Naye akaenda, akamkuta katika mlima wa Mungu, akambusu.

28. Musa akamwambia Haruni hayo maneno yote ya BWANA ambayo alimtuma aende nayo, na ishara hizo zote alizomwagiza.

29. Musa na Haruni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa watu wa Israeli.

30. Haruni akawaambia maneno yote BWANA aliyonena na Musa akazifanya zile ishara mbele ya watu.

31. Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa BWANA amewajilia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainama vichwa vyao wakasujudu.

Kut. 4