10. Nao wakatia safu nne za vito ndani yake, safu moja ilikuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, vilikuwa ni safu ya kwanza.
11. Na safu ya pili ilikuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi.
12. Na safu ya tatu ilikuwa ni hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto.
13. Na safu ya nne ilikuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi: vito hivyo vilikuwa vimetiwa katika vijalizo vya dhahabu, kila kimoja mahali pake.
14. Na hivyo vito vilikuwa vyaandama majina ya wana wa Israeli, kumi na mawili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora muhuri, kila moja kwa jina lake, kwa zile kabila kumi na mbili.
15. Nao wakafanya katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa ya dhahabu safi.
16. Nao wakafanya vijalizo viwili vya dhahabu, na pete mbili za dhahabu; nao wakazitia hizo pete mbili katika ncha mbili za hicho kifuko.
17. Nao wakaitia hiyo mikufu miwili iliyosokotwa katika hizo pete mbili zilizokuwa katika ncha mbili za hicho kifuko.
18. Na ncha hizo mbili nyingine, za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa, wakazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera, upande wa mbele.
19. Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani.
20. Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi.
21. Nao wakakikaza kile kifuko kwa pete zake kwenye naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kikae pale juu ya mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, na ya kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera; vile vile kama BWANA alivyomwagiza Musa.
22. Naye akafanya hiyo joho ya naivera ya kazi ya kusuka, rangi ya samawi yote;