Kut. 36:10-27 Swahili Union Version (SUV)

10. Naye akaunganisha mapazia matano hili na hili; na mapazia matano mengine akayaunganisha hili na hili.

11. Kisha akafanya matanzi ya rangi ya samawi katika ncha za pazia moja, katika upindo wa kiungo chake; akafanya vivyo katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili.

12. Akafanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililokuwa katika kiungo cha pili; hayo matanzi yalikuwa yakabiliana hili na hili.

13. Kisha akafanya vifungo hamsini vya dhahabu, na kuyaunganya hayo mapazia hili na hili kwa vile vifungo; hivi ile maskani ilikuwa ni moja.

14. Kisha akafanya vifuniko vya singa za mbuzi kuwa hema ya kuifunika hiyo maskani; akafanya mapazia kumi na moja.

15. Urefu wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa nne; hayo mapazia yote kumi na moja yalikuwa ya kipimo kimoja.

16. Naye akaunganya mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali.

17. Kisha akafanya matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililo upande wa nje katika kile kiungo, naye akafanya matanzi hamsini katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili.

18. Kisha akafanya vifungo hamsini vya shaba aiunganye ile hema pamoja, ili iwe hema moja.

19. Kisha akafanya kifuniko kwa ajili ya hiyo hema cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu; tena juu yake akafanya kifuniko cha ngozi za pomboo.

20. Kisha akafanya mbao za mti wa mshita kwa hiyo maskani, zilizosimama.

21. Urefu wa kila ubao ulikuwa ni dhiraa kumi, na upana wa kila ubao ulikuwa ni dhiraa moja na nusu.

22. Kila ubao ulikuwa na ndimi mbili, zilizounganywa pamoja; ndivyo alivyozifanya hizo mbao zote za maskani.

23. Naye akazifanya hizo mbao kwa ajili ya hiyo maskani; mbao ishirini kwa upande wa kusini kuelekea kusini;

24. naye akafanya matako ya fedha arobaini yawe chini ya hizo mbao ishirini; matako mawili chini ya ubao mmoja kwa hizo ndimi zake mbili, na matako mawili chini ya ubao mwingine kwa ndimi zake mbili.

25. Na kwa upande wa pili wa maskani upande wa kaskazini, akafanya mbao ishirini,

26. na matako yake ya fedha arobaini; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao mwingine.

27. Na kwa upande wa nyuma wa hiyo maskani kuelekea magharibi akafanya mbao sita.

Kut. 36