Kut. 36:1-17 Swahili Union Version (SUV)

1. Basi Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye BWANA amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote BWANA aliyoyaagiza.

2. Basi Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu, na kila mtu aliyekuwa na moyo wa akili, ambaye BWANA alimtia moyoni mwake hekima, kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza ili aende kuifanya kazi hiyo;

3. nao wakapokea mkononi mwa Musa matoleo yote, ambayo hao wana wa Israeli walikuwa wameyaleta kwa ajili ya huo utumishi wa mahali patakatifu, ili wapafanye. Kisha wakamletea matoleo kila siku asubuhi kwa moyo wa kupenda.

4. Na hao watu wote wenye hekima, waliotumika katika kazi yote ya mahali patakatifu, wakaenda kila mtu kutoka katika kazi yake aliyokuwa akiifanya;

5. nao wakasema na Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo BWANA aliagiza ifanywe.

6. Basi Musa akatoa amri, nao wakatangaza mbiu katika marago yote, wakisema, Wasifanye kazi tena, mtu mume wala mwanamke, kwa ajili ya matoleo kwa mahali patakatifu. Basi watu wakazuiwa wasilete tena.

7. Kwani vile vitu walivyokuwa navyo vilikuwa vyatosha kwa kuifanya kazi hiyo yote, kisha vilizidi.

8. Basi kila mtu mwenye moyo wa hekima miongoni mwa hao waliofanya kazi, akaifanya hiyo maskani ya mapazia kumi; ya nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu; pamoja na makerubi, kazi ya fundi stadi; ndivyo alivyoyafanya.

9. Urefu wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa nne; mapazia yote yalikuwa ya kipimo kimoja.

10. Naye akaunganisha mapazia matano hili na hili; na mapazia matano mengine akayaunganisha hili na hili.

11. Kisha akafanya matanzi ya rangi ya samawi katika ncha za pazia moja, katika upindo wa kiungo chake; akafanya vivyo katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili.

12. Akafanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililokuwa katika kiungo cha pili; hayo matanzi yalikuwa yakabiliana hili na hili.

13. Kisha akafanya vifungo hamsini vya dhahabu, na kuyaunganya hayo mapazia hili na hili kwa vile vifungo; hivi ile maskani ilikuwa ni moja.

14. Kisha akafanya vifuniko vya singa za mbuzi kuwa hema ya kuifunika hiyo maskani; akafanya mapazia kumi na moja.

15. Urefu wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa nne; hayo mapazia yote kumi na moja yalikuwa ya kipimo kimoja.

16. Naye akaunganya mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali.

17. Kisha akafanya matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililo upande wa nje katika kile kiungo, naye akafanya matanzi hamsini katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili.

Kut. 36