Kut. 34:7-18 Swahili Union Version (SUV)

7. mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne.

8. Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu.

9. Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako.

10. Akasema, Tazama, nafanya agano; mbele ya watu wangu wote nitatenda miujiza, ya namna isiyotendeka katika dunia yote, wala katika taifa lo lote; na watu wote ambao unakaa kati yao wataona kazi ya BWANA, kwa maana ni neno la kutisha nikutendalo.

11. Liangalie neno hili ninalokuamuru leo; tazama, mbele yako namtoa Mwamori, na Mkanaani, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.

12. Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako.

13. Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao.

14. Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa BWANA, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu.

15. Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake.

16. Ukawaoza wana wako binti zao, nao binti zao wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, wakawavuta wana wenu wafanye uzinzi na miungu yao.

17. Usijifanyizie miungu ya kuyeyusha.

18. Hiyo sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu utaitunza. Utakula mikate isiyotiwa chachu muda wa siku saba, kama nilivyokuagiza, kwa majira yaliyoaganwa katika mwezi wa Abibu; kwa kuwa ulitoka Misri katika mwezi huo wa Abibu.

Kut. 34