15. Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake.
16. Ukawaoza wana wako binti zao, nao binti zao wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, wakawavuta wana wenu wafanye uzinzi na miungu yao.
17. Usijifanyizie miungu ya kuyeyusha.
18. Hiyo sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu utaitunza. Utakula mikate isiyotiwa chachu muda wa siku saba, kama nilivyokuagiza, kwa majira yaliyoaganwa katika mwezi wa Abibu; kwa kuwa ulitoka Misri katika mwezi huo wa Abibu.
19. Kila kifunguacho mimba ni changu mimi; na wanyama wako wote walio waume, wazaliwa wa kwanza wa ng’ombe na wa kondoo.
20. Na mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; tena kwamba hutaki kumkomboa, ndipo utamvunja shingo. Wazaliwa wa kwanza wote wa wanao utawakomboa. Wala hapana atakayehudhuria mbele zangu mikono mitupu.
21. Utafanya kazi siku sita, lakini katika siku ya saba utapumzika; wakati wa kulima mashamba, na wakati wa kuvuna pia, utapumzika.
22. Nawe utaitunza sikukuu ya majuma, nayo ni ya malimbuko ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya vitu mwisho wa mwaka.
23. Mara tatu kila mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele za Bwana MUNGU, Mungu wa Israeli.
24. Kwa kuwa mimi nitazitupa nje taifa za watu mbele yako, na kuipanua mipaka yako; wala hapana mtu ye yote atakayeitamani nchi yako, hapo utakapokwea kwenda kuhudhuria mbele za BWANA Mungu wako mara tatu kila mwaka.