Kut. 30:6-21 Swahili Union Version (SUV)

6. Nawe utaitia mbele ya lile pazia lililo karibu na sanduku la ushuhuda mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, hapo nitakapokutana nawe.

7. Na Haruni atafukiza uvumba wa manukato juu yake; kila siku asubuhi atakapozitengeneza zile taa, ataufukiza.

8. Na Haruni atakapoziwasha zile taa wakati wa jioni, ataufukiza, uwe uvumba wa daima mbele za Bwana katika vizazi vyenu vyote.

9. Hamtafukiza juu yake uvumba mgeni, wala sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, wala hamtamimina juu yake sadaka ya kinywaji.

10. Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote; ni takatifu sana kwa BWANA.

11. BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

12. Utakapowahesabu wana wa Israeli, kama itakavyotokea hesabu yao, ndipo watakapompa BWANA kila mtu ukombozi kwa ajili ya roho yake, hapo utakapowahesabu; ili kwamba yasiwe maradhi kati yao, hapo utakapowahesabu.

13. Nacho watakachotoa ni hiki, kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa atatoa nusu shekeli kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu; (shekeli ni gera ishirini;) nusu shekeli kwa sadaka ya BWANA.

14. Kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa tangu huyo ambaye umri wake ni miaka ishirini, au zaidi, atatoa hiyo sadaka ya BWANA.

15. Matajiri hawataleta zaidi, wala maskini hawataleta kilichopungua, katika hiyo nusu shekeli, watakapotoa hiyo sadaka ya BWANA, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.

16. Nawe utapokea hizo fedha za upatanisho mikononi mwa hao wana wa Israeli, na kuziweka kwa ajili ya utumishi wa hema ya kukutania; ili kwamba ziwe ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli mbele ya BWANA, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.

17. BWANA akanena na Musa, na kumwambia

18. Fanya na birika la shaba, na tako lake la shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji.

19. Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo;

20. hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea BWANA sadaka ya moto;

21. basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote.

Kut. 30