17. BWANA akanena na Musa, na kumwambia
18. Fanya na birika la shaba, na tako lake la shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji.
19. Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo;
20. hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea BWANA sadaka ya moto;
21. basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote.
22. Kisha BWANA akasema na Musa, na kumwambia,
23. Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri nusu ya kiasi hicho, yaani, shekeli mia mbili na hamsini, na kane shekeli mia mbili na hamsini,
24. na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano;
25. nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa.
26. Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda,
27. na hiyo meza, na vyombo vyake vyote, na kinara cha taa, na vyombo vyake, na madhabahu ya kufukizia uvumba,
28. na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na tako lake.
29. Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu.