Kut. 30:1-8 Swahili Union Version (SUV)

1. Nawe fanya madhabahu ya kufukizia uvumba; utaifanyiza kwa mti wa mshita.

2. Urefu wake utakuwa dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; itakuwa mraba; na kwenda juu kwake dhiraa mbili; pembe zake zitakuwa za kitu kimoja nayo.

3. Nawe utaifunikiza dhahabu safi juu yake, na mbavu zake kando kando, na pembe zake; nawe utaifanyia ukingo wa dhahabu kuizunguka.

4. Kisha utaifanyia pete mbili za dhahabu, chini ya ukingo wake katika mbavu zake mbili, katika pande zake mbili utazifanya; nazo zitakuwa mahali pa kuitia miti ya kuichukulia.

5. Na ile miti utaifanya kwa mti wa mshita, na kuifunikiza dhahabu safi.

6. Nawe utaitia mbele ya lile pazia lililo karibu na sanduku la ushuhuda mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, hapo nitakapokutana nawe.

7. Na Haruni atafukiza uvumba wa manukato juu yake; kila siku asubuhi atakapozitengeneza zile taa, ataufukiza.

8. Na Haruni atakapoziwasha zile taa wakati wa jioni, ataufukiza, uwe uvumba wa daima mbele za Bwana katika vizazi vyenu vyote.

Kut. 30