13. Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu;
14. na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo.
15. Nawe utafanya kifuko cha kifuani cha hukumu, kazi ya fundi stadi; utakifanya kwa kuiandama ile kazi ya hiyo naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani safi yenye kusokotwa, ndivyo utakavyokifanya.
16. Kitakuwa mraba, tena cha kukunjwa; urefu wake utakuwa shibiri moja, na upana wake shibiri moja.
17. Nawe ukijaze viweko vya vito, safu nne za vito; safu moja itakuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, hivi vitakuwa safu ya kwanza;
18. na safu ya pili itakuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi;
19. na safu ya tatu itakuwa hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto;
20. na safu ya nne itakuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi; vito hivyo vitakazwa ndani ya dhahabu kwa kujaa mahali pake.
21. Na vile vito vitakuwa sawasawa na majina ya wana wa Israeli, kumi na viwili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora kwa muhuri kila kimoja sawasawa na jina lake, vitakuwa vya hizo kabila kumi na mbili.
22. Nawe utie katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa, ya dhahabu safi.
23. Nawe utie pete mbili za dhahabu katika kile kifuko cha kifuani, na kuzitia hizo pete mbili katika ncha mbili za kifuko cha kifuani.
24. Nawe utie hiyo mikufu miwili ya dhahabu iliyosokotwa katika zile pete mbili zilizo katika ncha za kifuko cha kifuani.