12. Nawe utavitia vile vito viwili juu ya vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli; naye Haruni atayachukua majina yao mbele za BWANA juu ya mabega yake mawili ili kuwa ukumbusho.
13. Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu;
14. na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo.
15. Nawe utafanya kifuko cha kifuani cha hukumu, kazi ya fundi stadi; utakifanya kwa kuiandama ile kazi ya hiyo naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani safi yenye kusokotwa, ndivyo utakavyokifanya.
16. Kitakuwa mraba, tena cha kukunjwa; urefu wake utakuwa shibiri moja, na upana wake shibiri moja.
17. Nawe ukijaze viweko vya vito, safu nne za vito; safu moja itakuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, hivi vitakuwa safu ya kwanza;