3. Na vyombo vyake vya kuyaondoa majivu yake utavifanya, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote utavifanya vya shaba.
4. Nawe uifanyie hiyo madhabahu wavu wa shaba; kisha utie pete nne za shaba katika hizo pembe nne za ule wavu.
5. Nawe tia huo wavu chini ya kizingo kiizungukacho madhabahu upande wa chini, ili huo wavu ufikilie katikati ya hiyo madhabahu.
6. Nawe fanya miti kwa ajili ya madhabahu, miti ya mshita, na kuifunika shaba.
7. Na hiyo miti itatiwa katika pete, na ile miti itakuwa katika pande mbili za madhabahu, wakati wa kuichukua.
8. Uifanye ya mbao, yenye mvungu ndani yake; kama ulivyoonyeshwa mlimani, ndivyo watakavyoifanya.
9. Nawe fanya ua wa maskani; upande wa kusini wa kuelekea kusini kutakuwa na chandarua ya nguo ya kitani nzuri yenye kusokotwa, kwa huo ua, urefu wake upande mmoja utakuwa ni dhiraa mia;
10. na nguzo zake zitakuwa nguzo ishirini, na matako yake ishirini, matako yake yatakuwa ya shaba; kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha.
11. Ni vivyo upande wa kaskazini, urefu wake hiyo chandarua utakuwa ni dhiraa mia, na nguzo zake ishirini, na matako yake ishirini yatakuwa ya shaba; kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha.
12. Na upande wa magharibi, upana wa ua kutakuwa na chandarua ya dhiraa hamsini; nguzo zake kumi, na matako yake kumi.
13. Na upana wa ule ua upande wa mashariki kuelekea mashariki utakuwa ni dhiraa hamsini.
14. Chandarua upande mmoja wa lango itakuwa dhiraa kumi na tano upana wake; nguzo zake zitakuwa tatu na matako yake matatu.