Kut. 26:21-36 Swahili Union Version (SUV)

21. na matako yake ya fedha arobaini; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao mwingine.

22. Kisha ufanye mbao sita kwa ajili ya upande wa nyuma wa maskani kuelekea magharibi.

23. Tena ufanye mbao mbili kwa ajili ya hizo pembe za maskani zilizo upande wa nyuma.

24. Upande wa chini zitakuwa ni mbili mbili; vivyo zitaungwa pamoja mbao pacha hata ncha ya juu katika pete ya kwanza; zote mbili ndivyo zitakavyokuwa; zitakuwa kwa ajili ya hizo pembe mbili.

25. Mbao zitakuwa ni nane, na matako yake ya fedha, matako kumi na sita; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao wa pili.

26. Nawe fanya mataruma ya mti wa mshita; mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa maskani,

27. na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa pili wa maskani, na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa maskani ulio nyuma kuelekea magharibi.

28. Na hilo taruma la katikati, lililo katikati ya zile mbao litapenya toka mwisho huu hata mwisho huu.

29. Na hizo mbao utazifunika dhahabu, na pete zake za kutilia yale mataruma utazifanya za dhahabu; na hayo mataruma utayafunika dhahabu.

30. Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake ulioonyeshwa mlimani.

31. Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi;

32. kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika matako ya fedha manne.

33. Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda na kulitia humo nyuma ya pazia; na lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana.

34. Nawe utaweka kiti cha rehema juu ya lile sanduku la ushuhuda ndani ya mahali pale patakatifu sana.

35. Na ile meza utaiweka nje ya pazia, na kinara cha taa kuikabili ile meza upande wa maskani wa kuelekea kusini; na ile meza utaiweka upande wa kaskazini.

36. Kisha utafanya kisitiri kwa mlango wa Hema, cha nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshona taraza.

Kut. 26