Kut. 25:20-31 Swahili Union Version (SUV)

20. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema.

21. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku.

22. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.

23. Nawe fanya meza ya mti wa mshita; urefu wake utakuwa dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu.

24. Uifunike dhahabu safi, na kuifanyia ukingo wa dhahabu wa kuizunguka pande zote.

25. Kisha ifanyie upapi wa kuizunguka pande zote, upana wake utakuwa nyanda nne, nawe uufanyie ule upapi ukingo wa urembo wa dhahabu wa kuuzunguka pande zote.

26. Uifanyie vikuku vinne vya dhahabu, na kuvitia vile vikuku katika pembe zake nne, katika miguu yake minne.

27. Vile vikuku na viwe karibu na ule upapi, ili viwe mahali pa kutilia ile miti, ya kuichukulia meza.

28. Fanya ile miti ya mti wa mshita, na kuifunika dhahabu, kwamba ile meza ichukuliwe kwayo.

29. Nawe fanya sahani zake, na miiko yake, na makopo yake, na vikombe vyake vya kumiminia; vifanye vyote vya dhahabu safi.

30. Nawe utaiweka mikate ya wonyesho juu ya meza mbele yangu daima.

31. Nawe fanya kinara cha taa cha dhahabu safi; hicho kinara na kifanywe cha kazi ya kufua, tako lake, na mti wake, vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vitakuwa vya kitu kimoja nacho;

Kut. 25