19. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku.
20. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema.
21. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku.
22. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.
23. Nawe fanya meza ya mti wa mshita; urefu wake utakuwa dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu.
24. Uifunike dhahabu safi, na kuifanyia ukingo wa dhahabu wa kuizunguka pande zote.