1. Kisha BWANA akamwambia Musa, Kweeni wewe, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini wa wazee wa Israeli, mkamfikilie BWANA; mkasujudie kwa mbali;
2. na Musa peke yake ndiye atakayekaribia karibu na BWANA; lakini hao hawatakaribia karibu; wala hao watu hawatakwea pamoja naye.
3. Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya BWANA, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena BWANA tutayatenda.
4. Basi Musa akayaandika maneno yote ya BWANA, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli,
5. akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia BWANA sadaka za amani za ng’ombe.