4. Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi.
5. Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu,
6. nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli.
7. Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, BWANA aliyokuwa amemwagiza.
8. Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema BWANA tutayatenda. Naye Musa akamwambia BWANA maneno ya hao watu.
9. BWANA akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako katika wingu zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa akamwambia BWANA hayo maneno ya watu.
10. BWANA akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao,
11. wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu BWANA atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote.
12. Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa.
13. Mkono wa mtu awaye yote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima.
14. Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao.