13. Ikawa wakati wa jioni, kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo.
14. Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi.
15. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle.
16. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.
17. Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua.
18. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa.
19. Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi.
20. Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana.
21. Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka.
22. Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa.
23. Akawaambia, Ndilo neno alilonena BWANA Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa BWANA; okeni mtakachooka, na kutokosa mtakachotokosa; na hicho kitakachowasalia jiwekeeni kilindwe hata asubuhi.
24. Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; nacho hakikutoa uvundo wala kuingia mabuu.
25. Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya BWANA; leo hamtakiona nje barani.