Kut. 15:19-27 Swahili Union Version (SUV)

19. Kwa maana farasi za Farao na magari yake na wapanda farasi wake waliingia ndani ya bahari, BWANA akayarudisha maji ya bahari juu yao; bali wana wa Israeli walikwenda katika nchi kavu katikati ya bahari.

20. Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza.

21. Miriamu akawaitikia,Mwimbieni BWANA kwa maana ametukuka sana;Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.

22. Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

23. Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara.

24. Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

25. Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko;

26. akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye.

27. Wakafikilia Elimu, palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na mitende sabini; wakapanga hapo, karibu na maji.

Kut. 15