Kut. 12:8-18 Swahili Union Version (SUV)

8. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu.

9. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani.

10. Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto.

11. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA.

12. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA.

13. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.

14. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele

15. Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba; siku hiyo ya kwanza mtaondoa chachu yote isiwe katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula mkate uliochachwa tangu siku hiyo ya kwanza hata siku ya saba, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na Israeli.

16. Siku ya kwanza kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na siku ya saba kutakuwa kusanyiko takatifu; haitafanywa kazi yo yote katika siku hizo, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu.

17. Nanyi mtaitunza ile sikukuu ya mikate isiyochachwa; kwa kuwa katika siku iyo hiyo mimi nimeyatoa majeshi yenu katika nchi ya Misri; kwa hiyo mtaitunza siku hiyo katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.

18. Mwezi wa kwanza, siku ya mwezi kumi na nne, wakati wa jioni, mtakula mikate isiyochachwa, hata siku ya mwezi ishirini na moja jioni.

Kut. 12