Kut. 12:38-51 Swahili Union Version (SUV)

38. Na kundi kubwa la watu waliochangamana mno wakakwea pamoja nao; na kondoo na ng’ombe, wanyama wengi sana.

39. Nao wakaoka mikate isiyochachwa ya ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana, haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri, wasiweze kukawia, nao walikuwa hawajajifanyia tayari chakula.

40. Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini.

41. Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya BWANA yalitoka nchi ya Misri.

42. Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za BWANA kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa BWANA, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao.

43. BWANA akawaambia Musa na Haruni, Amri ya pasaka ni hii; mtu mgeni asimle;

44. lakini mtumishi wa mtu awaye yote aliyenunuliwa kwa fedha, ukiisha kumtahiri, ndipo hapo atamla pasaka.

45. Akaaye kwenu hali ya ugeni, na mtumishi aliyeajiriwa, wasimle pasaka.

46. Na aliwe ndani ya nyumba moja; usiichukue nje ya nyumba nyama yake yo yote; wala msivunje mfupa wake uwao wote.

47. Na wafanye jambo hili mkutano wa Israeli wote.

48. Na mgeni atakapoketi pamoja nawe, na kupenda kumfanyia BWANA pasaka, waume wake wote na watahiriwe, ndipo hapo akaribie na kufanya pasaka; naye atakuwa mfano mmoja na mtu aliyezaliwa katika nchi; lakini mtu ye yote asiyetahiriwa asimle.

49. Sheria ni hiyo moja kwa mtu aliyezaliwa kwenu, na kwa mgeni akaaye kati yenu ugenini.

50. Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli wote; kama BWANA alivyowaagiza Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya.

51. Ilikuwa siku ile ile moja, BWANA akawatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri kwa majeshi yao.

Kut. 12