Kut. 10:7-17 Swahili Union Version (SUV)

7. Ndipo watumishi wa Farao wakamwambia, Mtu huyu atakuwa tanzi kwetu sisi hata lini? Wape hawa watu ruhusa waende zao, wamtumikie BWANA, Mungu wao; hujatambua bado ya kuwa Misri imekwisha haribika?

8. Musa na Haruni wakaletwa tena kwa Farao; naye akawaambia, Nendeni, mkamtumikie BWANA, Mungu wenu; lakini ni kina nani watakaokwenda?

9. Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng’ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia BWANA sikukuu.

10. Lakini akawaambia, Ehe, BWANA na awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu; angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu.

11. Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie BWANA; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni pa Farao.

12. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri kwa hao nzige, ili wakwee juu ya nchi ya Misri, waile mimea yote ya nchi, yaani, vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe.

13. Basi Musa akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri, na BWANA akaleta upepo kutoka mashariki juu ya nchi, mchana kutwa, na usiku kucha; kulipopambazuka ule upepo wa mashariki ukawaleta nzige.

14. Na hao nzige wakakwea juu ya nchi yote ya Misri, wakatua ndani ya mipaka yote ya Misri, walikuwa wabaya mno; hawajakuwapo nzige kama hao majira yo yote, wala baada yao hawatakuwa wengine jinsi hiyo.

15. Kwa kuwa waliufunika uso wote wa nchi, hata nchi iliingia giza; wakala mimea yote ya nchi, na matunda yote ya miti yaliyosazwa na ile mvua ya mawe; hapakusalia hata jani moja, mti wala mmea wa mashamba, katika nchi yote ya Misri.

16. Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni haraka; akasema, Nimemfanyia dhambi BWANA, Mungu wenu na ninyi pia.

17. Basi sasa, nawasihi, nisameheni dhambi yangu mara hii moja tu, mkamwombe BWANA, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki tu.

Kut. 10