15. Kwa kuwa waliufunika uso wote wa nchi, hata nchi iliingia giza; wakala mimea yote ya nchi, na matunda yote ya miti yaliyosazwa na ile mvua ya mawe; hapakusalia hata jani moja, mti wala mmea wa mashamba, katika nchi yote ya Misri.
16. Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni haraka; akasema, Nimemfanyia dhambi BWANA, Mungu wenu na ninyi pia.
17. Basi sasa, nawasihi, nisameheni dhambi yangu mara hii moja tu, mkamwombe BWANA, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki tu.
18. Akatoka kwa Farao, na kumwomba BWANA.
19. BWANA akaugeuza upepo wa magharibi wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka katika Bahari ya Shamu; hakusalia hata nzige mmoja ndani ya mipaka yote ya Misri.
20. Lakini BWANA akaufanya ule moyo wa Farao uwe mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa waende zao.
21. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, kuwe giza juu ya nchi ya Misri, watu wapapase-papase gizani.
22. Basi Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri muda wa siku tatu;
23. hawakupata kuonana mtu na mwenziwe, wala hakuondoka mtu mahali alipokuwa muda wa siku tatu; lakini wana wa Israeli wote walikuwa na mwanga makaoni mwao.
24. Farao akamwita Musa, na kumwambia, Haya, nendeni, mkamtumikie BWANA; kondoo zenu na ng’ombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi.