13. Basi Musa akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri, na BWANA akaleta upepo kutoka mashariki juu ya nchi, mchana kutwa, na usiku kucha; kulipopambazuka ule upepo wa mashariki ukawaleta nzige.
14. Na hao nzige wakakwea juu ya nchi yote ya Misri, wakatua ndani ya mipaka yote ya Misri, walikuwa wabaya mno; hawajakuwapo nzige kama hao majira yo yote, wala baada yao hawatakuwa wengine jinsi hiyo.
15. Kwa kuwa waliufunika uso wote wa nchi, hata nchi iliingia giza; wakala mimea yote ya nchi, na matunda yote ya miti yaliyosazwa na ile mvua ya mawe; hapakusalia hata jani moja, mti wala mmea wa mashamba, katika nchi yote ya Misri.
16. Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni haraka; akasema, Nimemfanyia dhambi BWANA, Mungu wenu na ninyi pia.
17. Basi sasa, nawasihi, nisameheni dhambi yangu mara hii moja tu, mkamwombe BWANA, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki tu.
18. Akatoka kwa Farao, na kumwomba BWANA.
19. BWANA akaugeuza upepo wa magharibi wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka katika Bahari ya Shamu; hakusalia hata nzige mmoja ndani ya mipaka yote ya Misri.