Kut. 10:10-26 Swahili Union Version (SUV)

10. Lakini akawaambia, Ehe, BWANA na awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu; angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu.

11. Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie BWANA; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni pa Farao.

12. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri kwa hao nzige, ili wakwee juu ya nchi ya Misri, waile mimea yote ya nchi, yaani, vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe.

13. Basi Musa akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri, na BWANA akaleta upepo kutoka mashariki juu ya nchi, mchana kutwa, na usiku kucha; kulipopambazuka ule upepo wa mashariki ukawaleta nzige.

14. Na hao nzige wakakwea juu ya nchi yote ya Misri, wakatua ndani ya mipaka yote ya Misri, walikuwa wabaya mno; hawajakuwapo nzige kama hao majira yo yote, wala baada yao hawatakuwa wengine jinsi hiyo.

15. Kwa kuwa waliufunika uso wote wa nchi, hata nchi iliingia giza; wakala mimea yote ya nchi, na matunda yote ya miti yaliyosazwa na ile mvua ya mawe; hapakusalia hata jani moja, mti wala mmea wa mashamba, katika nchi yote ya Misri.

16. Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni haraka; akasema, Nimemfanyia dhambi BWANA, Mungu wenu na ninyi pia.

17. Basi sasa, nawasihi, nisameheni dhambi yangu mara hii moja tu, mkamwombe BWANA, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki tu.

18. Akatoka kwa Farao, na kumwomba BWANA.

19. BWANA akaugeuza upepo wa magharibi wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka katika Bahari ya Shamu; hakusalia hata nzige mmoja ndani ya mipaka yote ya Misri.

20. Lakini BWANA akaufanya ule moyo wa Farao uwe mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa waende zao.

21. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, kuwe giza juu ya nchi ya Misri, watu wapapase-papase gizani.

22. Basi Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri muda wa siku tatu;

23. hawakupata kuonana mtu na mwenziwe, wala hakuondoka mtu mahali alipokuwa muda wa siku tatu; lakini wana wa Israeli wote walikuwa na mwanga makaoni mwao.

24. Farao akamwita Musa, na kumwambia, Haya, nendeni, mkamtumikie BWANA; kondoo zenu na ng’ombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi.

25. Musa akasema, Ni lazima utupe mikononi mwetu na wanyama wa dhabihu na wa sadaka za kuteketezwa, ili tupate kumchinjia BWANA Mungu wetu dhabihu.

26. Makundi yetu pia watakwenda pamoja nasi; hautasalia nyuma hata ukwato mmoja; kwa maana inampasa kutwaa katika hao tupate kumtumikia BWANA, Mungu wetu; nasi hatujui, hata tutakapofika huko, ni kitu gani ambacho kwa hicho inatupasa kumtumikia BWANA.

Kut. 10