1. BWANA akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao; kwa kuwa mimi nimeufanya moyo wake mzito, nipate kuzionyesha ishara zangu hizi kati yao;
2. nawe upate kusema masikioni mwa mwanao, na masikioni mwa mjukuu wako, ni mambo gani niliyotenda juu ya Misri, na ishara zangu nilizozifanya kati yao; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
3. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, na kumwambia, BWANA, Mungu wa Waebrania, asema hivi, Je! Utakataa hata lini kujinyenyekeza mbele zangu? Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie.
4. Au, kwamba wakataa kuwapa hao watu wangu ruhusa waende zao, tazama, kesho nitaleta nzige waingie ndani ya mipaka yako;
5. nao wataufunika uso wa nchi, mtu asipate kuona hiyo nchi; nao watakula mabaki ya hayo yaliyopona yaliyowasalia baada ya ile mvua ya mawe, watakula kila mti umeao kwa ajili yenu mashambani;
6. na nyumba zako, na nyumba za watumishi wako, na nyumba za Wamisri wote zitajawa na nzige; mfano wake baba zako wala baba za baba zako hawakuona, tangu siku walipoanza kuwapo juu ya nchi hata hivi leo. Basi akageuka na kutoka kwa Farao.
7. Ndipo watumishi wa Farao wakamwambia, Mtu huyu atakuwa tanzi kwetu sisi hata lini? Wape hawa watu ruhusa waende zao, wamtumikie BWANA, Mungu wao; hujatambua bado ya kuwa Misri imekwisha haribika?
8. Musa na Haruni wakaletwa tena kwa Farao; naye akawaambia, Nendeni, mkamtumikie BWANA, Mungu wenu; lakini ni kina nani watakaokwenda?
9. Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng’ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia BWANA sikukuu.
10. Lakini akawaambia, Ehe, BWANA na awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu; angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu.
11. Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie BWANA; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni pa Farao.
12. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri kwa hao nzige, ili wakwee juu ya nchi ya Misri, waile mimea yote ya nchi, yaani, vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe.