19. Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia BWANA kutaka kuwaangamiza. Lakini BWANA alinisikiza wakati huo nao.
20. BWANA akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo.
21. Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani.
22. Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia BWANA hasira.
23. Na wakati alipowatuma BWANA kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya BWANA, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiza sauti yake.
24. Mmekuwa na uasi juu ya BWANA tokea siku nilipowajua ninyi.
25. Ndipo nikaanguka nchi mbele za BWANA siku zile arobaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka nchi; kwa kuwa BWANA alisema atawaangamiza.
26. Nikamwomba BWANA, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu.
27. Wakumbuke watumwa wako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie upotofu wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao;
28. isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu BWANA hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowapa ahadi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, alivyowatoa nje ili kuwaua jangwani.
29. Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka.