Kum. 9:13-26 Swahili Union Version (SUV)

13. Tena BWANA akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu;

14. niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao.

15. Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili.

16. Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng’ombe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia aliyowaamuru BWANA.

17. Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu.

18. Nikaanguka nchi mbele za BWANA siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyokosa, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, kwa kumkasirisha.

19. Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia BWANA kutaka kuwaangamiza. Lakini BWANA alinisikiza wakati huo nao.

20. BWANA akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo.

21. Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani.

22. Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia BWANA hasira.

23. Na wakati alipowatuma BWANA kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya BWANA, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiza sauti yake.

24. Mmekuwa na uasi juu ya BWANA tokea siku nilipowajua ninyi.

25. Ndipo nikaanguka nchi mbele za BWANA siku zile arobaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka nchi; kwa kuwa BWANA alisema atawaangamiza.

26. Nikamwomba BWANA, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu.

Kum. 9