1. Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengewa kuta hata mbinguni,
2. watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki?
3. Basi jua siku hii ya leo kuwa BWANA, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia BWANA.
4. Usiseme moyoni mwako, BWANA, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia BWANA niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya BWANA awafukuza nje mbele yako.
5. Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya BWANA, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno BWANA alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.