Kum. 8:5-17 Swahili Union Version (SUV)

5. Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo BWANA, Mungu wako, akurudivyo.

6. Nawe uzishike amri za BWANA, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha.

7. Kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima;

8. nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali;

9. nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake yafukuka shaba.

10. Nawe utakula ushibe, utamshukuru BWANA, Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa.

11. Jihadhari, usije ukamsahau BWANA, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo.

12. Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake;

13. na makundi yako ya ng’ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka;

14. basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa;

15. aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu,

16. aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako.

17. Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo.

Kum. 8