Kum. 5:12-31 Swahili Union Version (SUV)

12. Ishike siku ya Sabato uitakase, kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru.

13. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote;

14. lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng’ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe.

15. Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa BWANA, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato.

16. Waheshimu baba yako na mama yako; kama BWANA, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na BWANA, Mungu wako.

17. Usiue.

18. Wala usizini.

19. Wala usiibe.

20. Wala usimshuhudie jirani yako uongo.

21. Wala usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba ya jirani yako, wala shamba lake, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala kitu cho chote alicho nacho jirani yako.

22. Haya ndiyo maneno ambayo BWANA aliwaambia mkutano wenu wote mlimani kwa sauti kuu toka kati ya moto, na wingu, na giza kuu; wala hakuongeza neno. Akayaandika juu ya mbao mbili za mawe, akanipa.

23. Ikawa, mlipoisikia sauti ile toka kati ya giza, na wakati uo huo mlima ule ulikuwa ukiwaka moto, basi, mlinikaribia, naam, wakuu wote wa kabila zenu, na wazee wenu,

24. mkasema, Tazama, BWANA, Mungu wetu, ametuonyesha utukufu wake, na ukuu wake, nasi tunasikia sauti yake toka kati ya moto; mmeona leo ya kuwa Mungu husema na mwanadamu, naye akaishi.

25. Sasa basi, mbona tufe? Maana moto huu mkubwa utatuteketeza; tukiisikia tena sauti ya BWANA, Mungu wetu, tutakufa.

26. Maana katika wote wenye mwili ni nani aliyeisikia sauti ya Mungu aliye hai, akisema toka kati ya moto, kama vile sisi, asife?

27. Enenda karibu wewe, ukasikie yote atakayoyasema BWANA, Mungu wetu; ukatuambie yote atakayokuambia BWANA, Mungu wetu; nasi tutayasikia na kuyatenda.

28. Naye BWANA akasikia sauti ya maneno yenu mliyoniambia; BWANA akaniambia, Nimesikia sauti ya maneno ya watu hawa waliyokuambia; wamesema vema yote waliyosema.

29. Laiti wangekuwa na moyo kama huu ndani yao sikuzote, wa kunicha, na kushika amri zangu zote sikuzote, wapate kufanikiwa wao na watoto wao milele!

30. Enda uwaambie, Rudini hemani mwenu.

31. Lakini wewe, simama hapa karibu nami, nami nitanena nawe sheria zote, na amri na hukumu, utakazowafunza, wapate kuzifanya katika nchi niwapayo kuimiliki.

Kum. 5