1. Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda.
2. BWANA, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu.
3. BWANA hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani, sisi sote tuliopo hapa, tu hai.
4. BWANA alisema nanyi uso kwa uso mlimani, toka kati ya moto;
5. (nami wakati ule nalisimama kati ya BWANA na ninyi, ili kuwaonyesha neno la BWANA; maana, mliogopa kwa sababu ya ule moto, wala hamkupanda mlimani); naye akasema,
6. Mimi ni BWANA, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.
7. Usiwe na miungu mingine ila mimi.
8. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi.